Chama cha wahasibu chataka Mashahidi wa kesi za ufisadi wapewe ulinzi

ANGAZO ATHMAN LUCHI  HITS: 201

Chama cha wahasibu nchini Kenya ICPAK kimeitaka idara ya mahakama kuhakikisha kuwa watu wanaodaiwa kuwa mashahidi katika kesi zinazohusisha ufisadi wa mali ya umma wamepewa ulinzi wa kutosha.

Mwenyekiti wa chama hicho Rose Mwaura amesema mara nyingi baadhi ya mashahidi katika kesi za ufisadi hususan wahasibu katika taasisi kuu za serikali huogopa kutoa ushahidi wao kwa kuhofia  maisha yao ikiwemo baadhi yao kutishwa maisha, kufutwa kazi, kupewa uhamisho na hata baadhi yao kupatikana wamefariki kwa njia za kutatanisha.

Amesema licha ya kipengee cha kuwalinda mashahidi kuwepo kwenye katiba, kipengee hicho kimekosa kuzingatiwa kikamilifu na kuwa hali hii imechangia pakubwa baadhi ya mashahidi kususia kujiwasilisha mahakamani hasa kesi za ufisadi zinazowahusisha watu wenye usemi mkubwa serikalini na hata katika jamii hali ambayo ameitaja kuwa imelemaza vita dhidi ya ufisadi nchini.

Wakati uo huo, mhasibu Rose amesema tayari wamewasilisha mswada katika bunge la kitaifa wa kuwekea mkazo ulinzi wa mashahidi akisema kuwa ukosefu wa usalama wa mashahidi usipopewa kipaumbele, kesi za ufisadi zitazidi kukawia mahakamani na hata baadhi kutupiliwa mbali.

Ameongezea kuwa iwapo mswada huo utapitishwa, utawapa uhuru baadhi ya mashahidi katika kesi tofauti wakiwemo baadhi ya wahasibu kuwa huru kufika mahakamani wanapohitajika.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *